WOSIA NI NINI? | SEHEMU YA I

Wosia ni nini?

Tangazo la Serikali Nambari 436 la mwaka 1963 ambalo linajumuisha sheria za kimila linatafsiriwa wosia kama:- “kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake kuonesha nia yake jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya kufa kwake”

 Aina za wosia:

 Zipo aina kuu mbili za wosia, ambazoo ni:

 • Wosia wa maandishi
 • Wosia wa mdomo.

 (i) Wosia wa maandishi

 Kwa mwosia anayejua kusoma na kuandika ni lazima wosia wake uwe katika maandishi. Wosia huu unatakiwa uandikwe kwa kalamu ya wino au kalamu isiyofutika au upigwe chapa.  Tarehe ya wosia ni muhimu hivyo iandikwe. 

Kwa mwosia anayejua kuandika na kusoma wanahitajika mashahidi wawili tu. Kwa mwosia asiyejua kuandika au kusoma mashahidi wake wawe wanne na wajue kusoma na kuandika.

Mwandishi wa wosia (Mwosia) aweke sahihi katika wosia. Kama mwosia hajui kusoma na kuandika aweke alama ya kidole gumba cha mkono wa kulia.  Mashahidi washuhudie sahihi au alama ya mwosia na wenyewe waweke sahihi zao kwenye wosia. 

Mwosia atataja mtu au watu ambao anapenda wasimamie ugawaji wa mali baada ya kifo chake.

 (ii) Wosia wa mdomo/maneno

 Wosia huu unapaswa kushuhudiwa na mashahidi wasiopungua wanne.  Watu wawili kati ya mashahidi hao wawe ni wa ukoo wa huyo mwosia; na wawili wanaweza kutoka nje ya ukoo wa mwosia. Wosia huo waweze kufutwa kwa kutoa wosia mwingine wa mdomo au kwa kutoa wosia wa maandishi. 

Mtu asiyejua kusoma na kuandika ndiye anayeweza kutoa wosia wa mdomo na akipenda kuandikiwa vile vile inaruhusiwa.

Mara nyingi wosia huchukuliwa na baadhi ya watu kama ni uchuro, ama hauna umuhimu kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuvuja kwa wosia. Fikra hizi sio sahihi na hazisaidii chochote kwani kuandika wosia sio sawa na kufungua mlango wa mauti bali ni kuhakikisha utashi wako unafuatwa katika kurithisha mali zako kwa watu unaofikiri wanastahili.

(iii) Faida za wosia

 •  Mwosia anapata fursa ya kufanya mgawo wa mali yake kwa kadri anavyotaka.
 • Mwosia anapata fursa ya kuamua ni nani awe msimamizi wa mirathi yake
 • Wosia huepusha ugomvi na kuimarisha amani miongoni mwa warithi na wanandugu halali.
 • Wosia ni chombo cha kuhakikisha kwamba urithi unakwenda kwa warithi halali.

 (iv) Nani Anaweza kutoa wosia

 Mtu yoyote mwenye umri wa kuanzia miaka kumi na nane na mwenye akili timamu.

 Sifa za Wosia halali:

 Wa maandishi:

 •  Mwandikaji awe amefikisha miaka kumi na nane.
 • Awe na akili timamu wakati anaandika  wosia huo.
 • Lazima iandikwe kwa wino au ipigwe chapa.
 • Ueleze bayana nani atakuwa msimamizi wa wosia.
 • Ueleze bayana nani ni warithi.
 • Lazima uthibitishwe na watu wawili ambao mwosia atawachagua mwenyewe.
 • Lazima uwe na tarehe na saini au alama ya kidole gumba kulia cha muandikaji na mashahidi.
 • Warithi hawatakiwi kuwa mashahidi.
 • Wosia ni siri hivyo uhalali wake uje wakati muandikaji ameshakufa.
 • Katika sheria ya mila, ni muhimu mke au wake wa muandikaji wakawa mashahidi.

 

Wa mdomo:

 •  Katika sheria ya kimila, kama wosia ni wa mdomo, ni lazima  ushuhudiwe na watu wanne,  wawili kati yao kutoka jamaa ya mwosia Wosia chini ya Sheria ya Serikali hauitofautiani na sifa hizo hapa juu ila wenyewe lazima uwe wa maandishi.
 •  Chini ya Sheria ya Kiislamu si ruhusa kugawa mali zaidi ya theluthi moja (1/3) ya mali yote ya mwosia kwa njia ya wosia.
 •  Wosia ugusie mali za marehemu tu. Wosia wowote ambao unarithisha mali zisizokuwa za marehemu au ambazo zilikuwa zinamilikiwa na marehemu pamoja na mtu mwingine kwa namna ya maslahi yasiyogawanyika wosia huo hautakuwa halali

Chini ya sheria ya mila wosia hautakuwa halali iwapo mashahidi wamekufa kabla ya mwosia hajafa, mali zitagawiwa kwa utaratibu kama usingekuwapo wosia.

Kubadili au kufuta wosia

Wosia waweza kubadilishwa au kufutwa na mwosia wakati wowote na iwapo umebadilishwa, ulioandikwa mwisho utachukuliwa kuwa umeibatilisha ule uliyoandikwa mwanzo.

 Sababu za Mtoa Wosia kumnyima mrithi, urithi

 • Kama mrithi alizini na mke wa mtoa wosia.
 • Kama mrithi alijaribu kumuua mtoa wosia au kumsababishia dhara la mwili au mama yake mtoa wosia.
 • Kama mrithi alidharau au alikataa kumtunza mtoa wosia katika shida ya njaa au ugonjwa.

 

KUMBUKA

Mtu atakaye kumnyima urithi au mrithi wake ni lazima aseme wazi katika wosia wake na aeleze sababu zake. Mrithi anayevunjiwa urithi apewe nafasi ya kujieleza mbele ya mtoa wosia au mbele ya Baraza la Ukoo na iwapo ataamua kunyamaza huku akijua kuwa amenyimwa urithi hawezi kupinga wosia baada ya kufa mwenye kutoa wosia.

 • Malalamiko yote yanayohusiana na urithi yatashughulikiwa na Baraza la Ukoo, na mtu anayehusika asiporidhika anaweza kulifikisha kwenye Baraza la hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.

 (v) Mahali pa kuhifadhi wosia

 Wosia waweza kutunzwa popote palipo pa usalama na ulinzi wa kutosha, ila kuepuka kughushi watu wengi huchagua kutunza katika sehemu zifuatazo;

 •  Kwenye vyombo vya kutoa msaada wa kisheria.
 • Asasi za kidini kama kanisa na msikiti
 • Kwa mwanasheria yeyote
 • Kwa mtu yeyote asiye mrithi katika wosia husika na ana sifa za kutunza siri.
 • Benki
 • Mahakamani

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

One thought on “WOSIA NI NINI? | SEHEMU YA I

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.