HakiElimu – Tuwakumbushe Viongozi wajao wasipuuze Elimu ya awali.

10533852_302712236576870_1789663602341715221_n

Mwaka huu watanzania tunafanya uamuzi wa kikatiba wa kuwachagua wawakilishi wetu katika ngazi mbalimbali zikiwemo udiwani, ubunge na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Wawakilishi hawa ndio ambao wataunda Serikali ya awamu ya tano ambayo pamoja na mambo mengine itaingia madarakani wakati taifa likitarajia mengi hasa kuboreshwa zaidi kwa elimu ya Tanzania na Utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Licha ya mijadala mizito inayoendelea kuhusu nani na nani wanafaa kuwa viongozi wetu, ni wazi kuwa wanahitajika watu wenye moyo thabiti wa kuinua kiwango cha elimu kuanzia awali hadi vyuo vikuu ambayo inakabiliwa na changamoto lukuki kiasi cha kuzua kejeli kwa wasomi wa taifa hili eti wengi wao ni wasomi vyeti ‘wasiouzika’ katika soko la ajira.

Serikali za awamu zote nne zimejitahidi kukabiliana na matatizo yanayoikabili sekta ya elimu,  umefika wakati kwa matatizo hayo kutokomezwa na kuondosha kabisa hali yoyote inayodhorotesha elimu.
Katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Serikali ilitambua  kuwa elimu ya awali ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na kimaadili. Cha kushangaza ni kwamba kuna uwekezaji duni wa rasilimali watu hasa walimu wa kuwanoa watoto, ukiachilia mbali miundombinu kama madarasa ambayo licha ya kujengwa, mengi ya madarasa hayo yanaonekana kuwa duni kiasi cha kutomvutia mtoto kufika shule kila siku.

Utafiti wa kihabari wa HakiElimu uliofanywa mwezi wa Agosti mwaka 2014 kuhusu ufahamu, uwekezaji na uwajibikaji kwenye elimu ya awali umeonyesha hali mbaya ya watoto wa awali kiasi cha kufundishwa na walimu walioitwa ‘wanakijiji’ wanaojitolea kwa nia njema ilihali hawana taaluma yoyote kuhusu malezi ama ufundishaji wa watoto wadogo ambao ndio kwanza wanaanza kuipanda ngazi ya elimu.
Vilevile Utafiti uliofanyika nchini katika miaka ya 1980, umebaini kuwa watoto waliopitia elimu ya awali huwa na mafanikio makubwa zaidi wanapoanza darasa la kwanza. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali iliamua kuingiza elimu ya awali kwa watoto wenye umri wa miaka mitano na sita kwenye mfumo rasmi wa elimu na kila shule ya msingi inapaswa kuwa na madarasa ya elimu ya awali.

Agizo hilo la kisera limetekelezwa kwa maana ya kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali. Hta hivyo, ubora wa madarasa na walimu ni suala jingine linalohitaji nia ya dhati ya viongozi na jamii kuamua kuifanya elimu ya awali kuwa kipaumbele kimojawapo cha taifa na kuzimaliza kabisa changamoto za elimu hii ya watoto ambao wanakatishwa tamaa na hali ya uduni wa mazingira na kuua kabisa vipaji na vipawa vyao ambavyo vilihitaji elimu kuendelezwa.
Tamko la HakiElimu kuhusu Bajeti ya sekta ya elimu mwaka wa fedha 2013/2014 iliweka wazi kuwa yanayotokea sasa katika sekta ya elimu yanaleta aibu kusimulia na yanaumiza kutafakari. Uwezo duni wa vijana wanaohitimu shule za msingi na sekondari, wanafunzi kufaulu bila kujua kusoma na kuandika, kuporomoka kwa ufaulu na kuongezeka kwa kiwango cha kutojua kusoma na kuandika.

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yanapaswa sasa kutufumbua macho na kutufanya tutambue ukweli kuwa tunapoteza mwelekeo na kama hatua za makusudi za kunusuru elimu zisipochukuliwa, basi tujue tunajenga Taifa la Watanzania wasio na ujuzi na maarifa ya kutatua changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazoendelea kutukabili.

Hadi mwaka 2012, takwimu za elimu zilionesha kuwa mazingira ya kujifunzia katika shule zetu kuanzia za awali mpaka sekondari hayakuwa ya kuvutia.

Kwa mfano, uwiano wa mwalimu mwenye sifa kwa mwanafunzi kwa elimu ya awali umebaki kuwa 1:124 badala ya 1:25 na hapa kimantiki ni aibu kwa kiongozi kujinadi atasaidia elimu endapo atashindwa hata kupambanua matatizo haya na kutafuta suluhu ya pamoja baina yake na jamii anayoiongoza.
Desemba 18, 2013, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Elimu ya Awali (TPTO), Mkoa wa Tanga, Prudence Charles alikaririwa na Gazeti la Mwananchi akiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutoa kipaumbele katika elimu hiyo na kusema ndicho chanzo cha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini. Alisema hakuna njia ya mkato zaidi ya kuwekeza katika elimu ya awali.

Pamoja na ukweli kuwa tunapozungumzia uboreshwaji wa elimu hasa ya awali tunapaswa kuwataja wadau wengi wa elimu ikiwemo jamii yenyewe, na asasi za kiraia serikali kama watunga sera na watekelezaji wakiwemo viongozi wa kisiasa hawawezi kukwema lawama hii.

Viongozi hawa pamoja na wale watakaochagulia na kuteuliwa kuunda serikali ya wamu ya tano wanapaswa kutambua kwamba  mzigo huu wa kutowekeza katika elimu ya awali unaligharimu taifa. Ni vyema kwa Rais ajaye atambue kuwa deni lake kwa wananchi ni kutoteua na kuwaweka madarakani watu wasio na tija hasa katika sekta nyeti ya elimu.

Kiongozi ambaye hawezi kuyatazama matatizo ya elimu na kuyamulika kwa jicho la utekelezaji na sio kwa matamko tu hafai kuwa kiongozi na inaweza kuwa sababu ya kumkataa kumpa dhamana ya uongozi katika taifa letu lenye raslimali za kutosha ambazo zinahitaji utashi na kuheshimu mawazo ya wadau na wananchi wa taifa hili.
Sera mpya ya elimu ya mwaka 2014 “Serikali imesema itaweka utaratibu wa elimu ya awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto   wenye umri kati ya miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja”.

Maneno haya yaliyomo kwenye sera yanahitaji watu makini wa kufikiri nje ya boksi na sio kuyasema maneno haya haya bali wawe sehemu ya kufanya kila linalowezekana hasa kuweka bajeti ya maana ya kuboresha elimu na sio kutumia kodi za watanzania kama posho na matumizi mengine.

Pamoja na mambo mengine sera hiyo inaweka wazi kuwa Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha muda wa kukamilisha elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu baada ya elimu msingi unalenga mwanafunzi  kupata ujuzi stahiki. Pia itahakikisha kuwa elimu msingi katika mfumo wa umma inatolewa “bila ada”.

Yote haya yanahitaji viongozi makini ambao hawatayaacha maneno haya kwenye makaratasi na kushinda majukwaani wakieleza changamoto badala ya kukabiliana nazo.

Imeandikwa Na Dennis Mwasalanga – HakiElimu.

Dennis Mwasalanga ni afisa Programu idara ya Habari na Utetezi HakiElimu
Na anapatikana katika barua pepe dennis.mboka@hakielimu.org

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.