Uchaguzi Mkuu 2015: Nani anastahili kura yako?

ROSE KALAGHE

Ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu wa 2015, kila raia wa Tanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 na aliyejiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, atatakiwa kushiriki katika kuwachagua viongozi mbalimbali katika ngazi za Urais, Ubunge na Udiwani. Viongozi watakaochaguliwa wanatarajiwa kuliongoza taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kupiga kura ni haki ya msingi ya kikatiba kwa kila raia wa Tanzania, ilimradi awe ametimiza matakwa ya kisheria. Katika nchi ya kidemokrasia kama Tanzania, upigaji kura ni kitendo muhimu sana kwani hutoa nafasi kwa umma kuchagua wawakilishi wao ndani na nje ya serikali. Hivyo ni muhimu sana kwa mwananchi kuwa na uhakika kuwa kiongozi anayechagua  ndiye kweli angependa amuongoze.

Kabla ya uchaguzi kufanyika, wagombea hujitokeza kupiga kampeni ili kuwaeleza wananchi makusudio na matarajio yao katika nafasi na majukumu wanayotarajia kukabidhiwa iwapo watashinda. Wagombea hutumia nafasi hiyo pia kuelezea mipango yao, pamoja na sera za vyama vyao. Aghalabu hutumia fursa hiyo kuahidi mambo watawayofanyia wapiga kura wao pindi watapochaguliwa.
Kipindi hiki cha kampeni, hugubikwa na mijadala na ahadi za wagombea na jinsi wanavozifahamu changamoto zinazoikabili jamii.

Mijadala hii  huambatana na na ahadi lukuki kuhusu namna watakavyotatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi  katika sekta za afya, elimu,  kilimo, maji, miundombinu n.k. ili kuleta maendeleo. Nguvu nyingi na rasilimali nyingi  hutumiwa na wagombea  kujinadi ili wachaguliwe.

Kwa bahati mbaya baada ya kuchaguliwa aghalabu wagombea wengi hushindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi  na hivyo kuwaacha wananchi katika  matatizo na kero nyingi.  Ndiyo maana wananchi wanapaswa kuwa makini wakati taifa linapoelekea kipindi cha uchaguzi. Mwananchi unapaswa  kuwa na orodha ya vigezo vya mtu unayetaka aje kukuongoza. Pamoja na vigezo vingine, atapaswa aoneshe nia  thabiti ya kuleta mabadiliko chanya, hasusani katika sekta ya elimu.

Kiongozi ajaye anapaswa kutambua changamoto zinazoikabili sekta  ya elimu na pia afahamu maana hasa ya elimu bora. Tunasisitiza zaidi suala la elimu kwani elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani kwani ili taifa liendelee  linahitaji wataalamu wenye ujuzi na stadi mbalimbali. Wataalamu hawa wanaweza kupatikana tu endapo, elimu inayotolewa ni bora na inakidhi mahitaji  ya nchi husika.
Mgombea huyo  lazima atambue kuwa elimu ni silaha muhimu katika maendeleo ya nchi kwani  inamuwezesha mtu mmoja mmoja kupambana na mazingira yake na hivyo kujiletea maendeleo kwa kuongeza uzalishaji iwe kwenye kilimo, uvuvi,  ufugaji na hata biashara.  Aiodha, elimu inasaidia aliye nayo kuondoa utegemezi wa kifikra na hata kihali na pia  humfanya ajiamini na huchochea hamu ya kuleta mabadiliko chanya katika  jamii.

Mgombea anayestashili kupigiwa kura sharti ajue kuwa hali ya elimu nchini hairidhishi na kwamba kwa sasa hakuna usawa katika utoaji wa elimu nchini kwani wenye uwezo wanawapeleka watoto wao kwenye shule nzuri, zenye walimu bora na vifaa, wakati watoto wa walalahoi, haswa vijijini, wanaendelea kupata elimu duni kwenye shule za umma. Suala la mlundikano wa wanafunzi darasani, uhaba wa waalimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, bajeti finyu, ukosefu wa sera nzuri ya elimu, ni baadhi tu ya changamoto zinazoathiri ubora wa elimu yetu.
Mwananchi kabla ya kupiga kura, ni vyema utambue kuwa taifa linahitaji viongozi wabunifu  watakaoliongoza  taifa hili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025, ambayo moja ya malengo yake ni kuwa na jamii iliyoelimika na yenye kujifunza, yenye ukomavu wa  fikra,  yenye kujiamini na yenye malengo thabiti ya kuleta maendeleo  kwa watanzania wote.

Tumeshuhudia awamu mbalimbali za uongozi katika nchi yetu  na  namna ambavyo viongozi katika awamu hizi wamelishughulikia suala zima la elimu. Hivi karibuni, tumeshuhudia mabadiliko mbalimbali katika sekta ya elimu, kama vile ubadilishwaji wa mara kwa mara wa mitaala na hata katika viwango vya ufaulu na utaratibu wa kutunuku matokeo ya kidato cha nne na sita. Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko ya aina hii yamechangia kuididimiza elimu yetu hasa kwa sababu mara nyingi huja bila maandalizi ya kutosha, hususani kwa upande wa rasilimali watu na vifaa.

Historia inaonesha kwamba elimu yetu ilikuwa na ubora wa hali ya juu miaka ya mwanzo ya uhuru wetu. Hii ni kwa sababu wakati ule viongozi walikuwa na nia thabiti ya kuisimamia elimu yetu. Kila kiongozi aliwajibika kuhakikisha kwamba malengo ya elimu nchini yanafikiwa. Lakini sasa hali ni tofauti kabisa kwani elimu yetu imeachwa tu; haina mwenyewe!

Kiongozi anayestahili kura yako sharti awe na sifa za uadilifu na uchapakazi.Aidha,  awe atayewajibika kuisimamia na kuilinda elimu yetu kwa manufaa yetu na nchi yetu kwani elimu bora ndiyo njia pekee ndiyo itakayomwezesha mtanzania na taifa kwa jumla kuondokana na umaskini uliokithiri.Bila kuwa na viongozi bora elimu bora ni ndoto.

Imeandikwa na Rose Kalaghe – HakiEimu

Rose Kalage  ni Afisa Programu katika Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera, Shirika la HakiElimu.

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.