Utafiti: Wanakwenda Shule lakini hawajifunzi

kusoma
Mwanafunzi akipimwa uwezo wa kusoma na kuhesabu katika moja ya tafiti za Uwezo.

Serikali imekuwa ikifanya mstari wa mbele kuhakikisha kwamba inaboresha elimu ya Tanzania. Wazazi nao wanaitikia vizuri wito wa elimu kwa kuwapeleka watoto wao shule

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo za  Serikali kama vile kujenga  shule, maabara na maktaba, kuajiri walimu wapya, kuanzisha sera mpya ya elimu, kuboresha mitalaa na mazingira ya kujifunzia, bado elimu ya Tanzania ina hali mbaya.

Hali hiyo imedhihirika kwenye utafiti mpya uliofanywa na asasi ya Twaweza kati ya mwaka 2013/14. Utafiti huo umebaini kuwa watoto saba kati ya 10 wa darasa la tatu hawana uwezo wa kufaulu mtihani wa darasa la pili.

Je, watoto wetu wanajifunza? Hilo ndiyo swali lililobeba dhima ya utafiti huo uliolenga kupima uwezo wa watoto katika kusoma na kuhesabu. Utafiti wa Twaweza umebaini kuwa nusu ya watoto wa darasa la tatu (asilimia 55) hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili.

Pia,  watoto nane kati ya 10 (asilimia 81) hawawezi kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha darasa la pili, wakati watoto wengine saba kati ya 10 wakiwa hawana uwezo wa kufanya kwa usahihi hesabu za kuzidisha za darasa la pili.

Mtafiti wa Twaweza, Richard Temu anasema utafiti huo ulifanyika katika wilaya 133, na watoto 104,162 wenye miaka kati ya saba na 16  walifanyiwa jaribio hilo.

Anasema asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka saba walikuwa wameandikishwa darasa la kwanza na kulikuwa hakuna pengo kati ya watoto wa kike na wa kiume waliokuwa wameandikishwa.

Elimu ya wazazi ina mchango

Hata hivyo, Temu anabainisha kuwa kulikuwa na pengo kubwa kati ya watoto ambao mama zao wana elimu na wale wasio na elimu.

 Alisema asilimia 48 ya watoto wa darasa la tatu na la nne ambao mama zao hawajasoma kabisa ndiyo walikuwa na uwezo wa kusoma na kufanya hesabu.

Asilimia 54 ya watoto wa darasa la tatu na la nne ambao mama zao wana elimu ya msingi na sekondari walikuwa na uwezo wa kusoma, wakati asilimia 73 ya watoto hao ambao mama zao wana elimu ya juu (zaidi ya kidato cha nne), waliweza kusoma na kuhesabu.

“Ule usemi kwamba ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima, hapa ndiyo unajidhihirisha wazi. Tunaona kama mama ana elimu ya kutosha, watoto wake pia watakuwa na nafasi kubwa ya kujifunza,” anasema mtafiti huyo.

Hali ya maisha ya wazazi

Temu anaeleza kuwa kuna tofauti kubwa ya uwezo wa kusoma na kuhesabu kwa watoto tajiri na masikini. Anasema asilimia 57 ya watoto tajiri wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili ukilinganisha na asilimia 40 ya watoto masikini.

Anasema asilimia 35 ya watoto tajiri wanaweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili ukilinganisha na asilimia 20 ya watoto masikini. Anaongeza kuwa asilimia 46 ya watoto tajiri wanaoweza kufanya hesabu za kuzidisha za darasa la pili ukilinganisha na asilimia 31 ya watoto masikini.

“Kwa jumla hali ya kujifunza kwa watoto ni mbaya nchini licha ya ukweli kuwa Serikali inajitahidi kujenga shule, kuajiri walimu wengi na kuongeza kiwango cha uandikishaji wa watoto. Serikali ina wajibu wa kufuatilia suala hilo kwa umakini ili kujua tatizo liko wapi,” anasema.

Naye Meneja wa programu ya Uwezo iliyo chini ya Twaweza, Zaida Mgalla, anasema ripoti hiyo inatoa fursa kwa wadau mbalimbali kujua hali halisi ya elimu nchini na kushiriki katika kuleta mabadiliko. Anasema Serikali imekuwa ikizipokea vizuri ripoti zao na kuzifanyia kazi.

“Serikali pekee haiwezi kuleta mabadiliko kwenye elimu ya Tanzania. Lazima wadau mbalimbali washiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ili watoto wajifunze kwa ufasaha,” anasema na kusisitiza kuwa sekta binafsi ina wajibu huo.

Anabainisha kuwa watoto hawapati maarifa muhimu ya mwanzo yatakayowawezesha kuwa na uelewa mzuri. Anawataka wadau kuchukua hatua za haraka ili kuinusu elimu ya Tanzania ambayo kwa sasa inaonekana kuwa na udhaifu mkubwa.

Mdau wa elimu, Godlisten Moshi anahoji juu ya uwezo wa walimu katika kufundisha wanafunzi. Anaeleza wasiwasi wake kuwa pengine walimu wanaofundisha wanafunzi hao, hawana uwezo wa kutosha kufanya kazi hiyo na ndiyo maana wanafunzi wengi wanashindwa kuwa na uelewa wa stadi hata zile za msingi.

“Serikali ielekeze nguvu katika kutoa mafunzo mazuri kwa walimu ili nao wawe na uwezo wa kufundisha wanafunzi kwa weledi. Kwa mfano, walimu wengi pia hawana ujuzi wa lugha ya Kiingereza, hivyo wanashindwa kuwafundisha watoto vizuri wakawaelewa,’’ anaeleza.

Mzazi mwenye watoto wa shule ya msingi, John Mwasaka anasema utafiti huo unatisha, kwa sababu elimu pekee ndiyo urithi wa mtoto. Anasema ni jukumu la wazazi wa watoto hasa wanaosoma shule za Serikali kufuatilia maendeleo ya watoto wao wawapo nyumbani.

“Serikali ichukue hatua ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu, ninasikia pia baadhi ya maeneo watoto wanamaliza darasa la saba bila kujua kusoma, kuandika wala kuhesabu,” anasisitiza mzazi huyo.

 

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.