Jaffar: Naamini Ufaulu Wangu Utanipeleka Ikulu

Mwanafunzi bora wa kwanza kitaifa, Jaffar Matange akipongezwa na mama yake, Halima Matange nyumbani kwao, baada ya matokeo ya daraza la saba kutangazwa wiki iliyopita. Picha na Salim Shao
Mwanafunzi bora wa kwanza kitaifa, Jaffar Matange akipongezwa na mama yake, Halima Matange nyumbani kwao, baada ya matokeo ya daraza la saba kutangazwa wiki iliyopita. Picha na Salim Shao

Ni Jumamosi ya Oktoba 31, siku ambayo Jaffar Matange(13) ameandika historia katika maisha yake na kuingia kwenye rekodi ya kitaifa.

Jaffar, mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wawili ameandika historia hiyo baada ya Baraza la Mitihani Tanzania kumtangaza ni mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015, uliofanyika Septemba.

Katika matokeo hayo, Jaffar ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Kimataifa Hazina, anatajwa kupata ufaulu wa juu zaidi akiwa na alama A katika masomo yote.

Ufaulu huo unamfanya kuwa kinara na kushika namba moja kati ya wanafunzi 775,273 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Darasa la Saba mwaka huu.

Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo mwandishi wa makala haya alimtafuta Jaffar na kufanikiwa kufanya mahojiano naye nyumbani kwao Ubungo Makoka, jijini Dar es Salaam.

Vifijo na nderemo vilitawala ndani ya nyumbani ya wazazi wa Jaffar, watu wakifurahia matokeo hayo yaliyomfanya Jaffar kung’ara na kuleta heshima kwa shule yake hata familia pia.

Akiwa na sura ya uchangamfu, Jaffar anaonekana kutawaliwa na tabasamu akishindwa kuficha furaha yake.

“Nimefurahi sana, najisikia raha kupita kiasi. Siku zote nilijua nitaingia kwenye kumi bora, lakini sikutegemea kama ningekuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa.

Nilikuwa namwambia mama nitafaulu na kama Rais atakayechaguliwa atakuwa na utaratibu wa kuwaita Ikulu wanafunzi 10 bora, basi lazima na mimi nitakuwepo, sijui kama mama alikuwa ananielewa,” anasema Jaffar akikumbuka kauli aliyoitoa kwa mama yake baada ya kufanya mtihani wa taifa.

Kama Rais Magufuli atakuwa na utaratibu huo basi ndoto ya Jaffar ya kuingia ikulu itakuwa imetimia.

Ilikuwaje akashika nafasi ya kwanza?

Jaffar anasema pamoja na kutulia na kusoma maswali kwa makini siku zote amekuwa akimtanguliza Mungu kwa kila analofanya.

“Mungu ndiyo kila kitu katika maisha yangu, siku zote namtanguliza yeye na ndiye aliyeniwezesha kufikia mafanikio haya hata leo nchi nzima imeweza kunitambua,” anasema.

Jaffar hakuacha kuwakumbuka walimu wake akisema wamekuwa na mchango mkubwa kwa hatua ya mafanikio aliyofikia, kwani walimfundisha kujiamini na kutulia wakati wa mitihani.

Anasema msimamo thabiti na ukali wa wastani waliokuwa nao walimu dhidi yao uliwafanya wanafunzi kujituma kupita kiasi hali iliyoibua ushindani wa hali ya juu darasani kwao.

“Tulikuwa tunachuana darasani, usitegemee ukiwa namba moja utaendelea kushika nafasi hiyo kila muhula, hivyo inakubidi usome kwa bidii ili ufanye vizuri, kinyume cha hapo ujiandae kwa kuchapwa,” anasema.

Jaffar anaongeza: “Kwa kuhofia kuchapwa, wanafunzi wote tulikuwa tunahangaika kufanya vizuri, ndiyo maana siyo kitu cha ajabu kwa shule yetu kuongoza katika Mkoa wa Dar s Salaam na kutoa wanafunzi bora kitaifa.”

Anataka kuwa nani?

Anasema lengo lake siku moja awe amebobea kwenye sayansi hasa katika masuala ya dawa za binadamu.

“Tayari nimeshafanya usaili na nimepata Shule ya Sekondari Feza, natarajia kujikita zaidi kwenye masomo ya sayansi kwa kuwa nayapenda mno. Namwomba Mungu aendelee kuwa nami katika masomo yangu ili niweze kufanya vizuri na kutimiza ndoto zangu,” anasema Jaffar.

Wazazi wanasemaje?

Halima Matange ni mama mzazi wa mwanafunzi huyo bora, anakiri Jaffar amekuwa akimweleza kuhusu ndoto yake ya kwenda Ikulu kwa kuingia katika kundi la kumi bora.

“Hata nashindwa kuelewa kwa nini alikuwa alijiamini hivyo, alikuwa akiniambia mama usiwe na wasiwasi kwenye 10 bora nipo na kama Rais mpya atawaita wanafunzi Ikulu yeye atakuwa mmoja wao.

Sikuyatilia maanani maneno hayo, ingawa aliniambia mara kwa mara. Nilitambua ana uwezo mzuri kichwani kwa sababu hata walimu wake walikuwa wakinipa taarifa,” anasema Halima.

Anaeleza kwamba tangu utoto Jaffar amekuwa akipenda kujifunza na siku zote masomo yamekuwa kipaumbele chake.

“Pamoja na kupenda kuangalia katuni, huwezi kumkuta amekaa kwenye runinga kabla hajamaliza kazi zake za darasani, hata anapoangalia katuni pembeni yake lazima kuna kitabu au daftari anasoma.

“Kifupi naweza kusema sikupata tabu na mtoto huyu ya kumlazimisha kusoma tangu alivyokuwa mdogo. Anajielewa na alionyesha kupenda shule tangu awali,” anasema.

Anasma tabia hiyo ilikuwa chachu kwa wazazi kwao wazazi kwani iliwalazimisha kufanya kila linalowezekana ili kumpa morali ya kufanya vizuri zaidi.

Kauli ya mwalimu

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kimataifa Hazina alipohitimu Jaffar darasa la saba, Patrick Cheche anasema walimu walitegemea ufaulu wa kijana huyo kutokana na maandalizi mazuri waliyopata wanafunzi wote.

Anasema pamoja na shule hiyo kutoa mwanafunzi wa kwanza na wa pili kwenye kumi bora kitaifa, pia imeweka rekodi ya kuwa na matokeo mazuri zaidi kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Tunajitahidi kuingiza walimu wenye viwango na ubora unaostahili na kila mmoja kwa nafasi yake anajitahidi kufundisha kwa maarifa yote ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri.

Mtindo wa kuwashindanisha wanafunzi katika masomo mbalimbali ulizidi kuleta ushindani na kuwafanya wajitume zaidi,” anasema Cheche.

Anamwelezea Jaffar kwamba ni mwanafunzi aliyekuwa akionyesha matumaini kwa muda mrefu wakati akichuana na wanafunzi wenzake darasani.

“Ufaulu wa Jaffar haukutushangaza sana kwani ni mtoto msikivu na anaelewa kwa haraka kila anachoelekezwa,” anasema.

Karim Seyn mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili kitaifa ambaye pia anatokea Shule ya Kimataifa Hazina, anasema jitihada na utulivu ndiyo zilizowawezesha yeye na Jaffar kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo.

“Kikubwa, walimu walitusisitiza kutulia na kusoma maswali kwa makini, siri hiyo ndiyo iliniwezesha binafsi kufanya vizuri, nilijitahidi kujizuia nisiwe na hofu.

“Tulikuwa na ushindani mkubwa darasani na wote tulijua tutafanya vizuri lakini mwenzangu amefanikiwa kuweka rekodi nafurahi kwa kuwa namba moja na namba mbili wote tumetoka Hazina,” anaeleza.

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.