Mchango wa Ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto katika Bajeti ya Wizara ya Elimu 2016/17

10930067_571818096282561_3761350164147276924_n
Mheshimiwa Spika, Mnamo Tarehe 9 Machi 1967 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa Chapisho la falsafa ya Elimu ya kujenga Nchi ya Kijamaa. Falsafa hii ni Elimu ya Kujitegemea ambayo ilitaka kuleta mapinduzi ya Elimu katika nchi yetu.

Mwalimu Nyerere alisema shabaha ya Elimu ni kutafsiri maarifa na busara kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kinachofuata na kuwaandaa vijana kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.


Falsafa hii ililenga kutatua changamoto za kutoa elimu yenye ubora tofauti kwa watu tofauti kulingana na kipato chao.

Falsafa ya Elimu ya Kujitegemea ililenga kuondoa ugandamizwaji wa wenye nguvu dhidi ya wanyonge na matajiri dhidi ya masikini.
Miaka karibia Hamsini sasa, tujiulize, Mfumo wetu waElimu unatoa maarifa mwafaka kwa vijana wetu?

Mfumo wetu wa Elimu unaondoa matabaka katika nchi yetu? Ni dhahiri kwamba hivi sasa tuna Elimu kwa ajili ya watu masikini na Elimu kwa ajili ya watu wenye uwezo. Tuna Elimu kwa ajili ya sisi viongozi na Walimu kwa ajili ya wapiga kura.


Mfumo wetu wa Elimu unajenga matabaka ya walionacho na wasionacho na kutokana na hali hiyo Serikali sasa inaanza hata kutaka kudhibiti bei za Shule binafsi ili wenye uwezo wasipandishiwe bei zikawa kubwa zaidi hasa baada ya Serikali mpya kubana mianya ya kupata mapato yasiyo halali kuwezesha kulipa ada kubwa.

Kazi ya Serikali kimsingi ni kusaidia wanyonge wanaosoma kwenye mashule yenye hali mbaya sana.


Mheshimiwa Spika, ifike wakati sasa tujiulize maswali magumu kuhusu Elimu. Tujiulize changamoto za Elimu ya Tanzania nini? Ni suala la Bajeti ndogo?

Ni suala la ubora wa Elimu? Kama ni kuhusu Bajeti ni kwanini uwekezaji mkubwa uliofanywa kwa miaka 10 ya Serikali ya awamu ya Nne ambapo zaidi ya tshs 2 trilioni zimewekwa kwenye Elimu haujaboresha Elimu yetu?

Kama ni kuhusu ubora ni kwanini tumeshindwa kulitatua na kila siku tunarudia na kurudia na kurudia? Ni nini NYUFA katika mfumo wetu wa Elimu wa sasa?


Ni dhahiri tumekuwa tukitoa majawabu yale yale kwa tatizo la ubora wa Elimu tukitegemea matokeo tofauti. Tumekuwa tukilalamika kuhusu Bajeti, Bajeti iliwahi kufika 20% ya Bajeti mwaka 2008 lakini hakuna kilichobadilika.

Tumekuwa tukilalamika kuhusu ughali wa Elimu na tukapanua udahili kwa kiwango kikubwa lakini bado shida za elimu zipo pale pale.


Hata sasa tumetangaza Elimu Msingi bila malipo na tunatuma fedha yote kwenye mashule (capitation grants), udahili umeongezeka kwenye baadhi ya maeneo mpaka 140%. Lakini Elimu bado haitengemai.


Mheshimiwa Spika, jana niliuliza rafiki zangu kwenye mtandao wa Facebook kuhusu mambo gani wanayotaka kufanywa ili kuboresha Elimu nchini kwetu. Nimeambatanisha maoni yao na kuwasilisha kwako ili yaingie kwenye hansards za Bunge.

Maoni mengi yanashabihiana na hali halisi ya Elimu yetu. Kila Mtanzania analalamika na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Elimu.


Mheshimiwa Spika, tumetunga Sera mpya ya Elimu inayounganisha elimu ya sasa ya Msingi na Sekondari na kuitwa Elimu Msingi. Tumeweka miaka 10 ya Watoto kusoma Elimu Msingi.

Mwono wa Sera ni kana kwamba changamoto zetu ni miaka ambayo watoto wanakaa shule.

Mwandishi mmoja kuhusu Elimu kaandika Kitabu The Rebirth of Education: Schooling isn’t Learing.

Mwandishi huyu anaitwa Lant Pritchett. Naomba watu wote wanaopenda Elimu nchini na wanaotaka kuleta mapinduzi kwenye elimu wasome kitabu hiki.


Kimsingi Pritchett anasema ‘kukaa darasani sio kupata elimu’.Kwenye nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, tumewekeza kwenye kufikia malengo ya idadi ya watoto wanaoandikishwa badala ya kuwekeza kwenye kutoa maarifa kwa watoto.

Ndio maana hapa nchini kwetu takribani vijana 60% wanaofanya mtihani wa kidato cha Nne hufeli kwa kupata sifuri na kwenye baadhi ya mikoa kama Kigoma 86% hupata sifuri na daraja la nne.

Watoto wanakwenda shuleni lakini hawajifunzi. Hawapati Elimu. Sera ya Elimu lazima itoe fursa ya kuzalisha watoto wanaopata elimu na sio kukaa darasani tu.


Utafiti wa karibuni kabisa unaonyesha ni 40% pekee ya watoto wa Darasa la Nne wanaoweza kufanya hesabu hii: 6 gawanya kwa 3 (6/3) au kuzidisha 7 x 8!

Matokeo ya miaka na miaka ya Uwezo yanaonyesha hali hiyo pia. Kwa mfano karibu asilimia 50% ya watoto wanaomaliza darasa la saba hawawezi kufanya mahesabu au kusoma hadithi ya darasa la tatu. Kwanini Watoto wetu hawajifunzi?


Mheshimiwa Spika, visababishi vya hali hii ni vingi sana. Lakini kikubwa kuliko vyote ni Mwalimu. Matatizo kuhusu Mwalimu Tanzania ni lundo lakini tunaweza kuongelea mawili kwa leo.


Mheshimiwa Spika, Uwepo wa walimu, katika miaka ya karibuni nchi yetu imepiga hatua katika kusomesha na kusambaza walimu.

Lakini walimu wengi waliopo mashuleni hawafundishi. Utafiti wa karibuni kabisa unaonyesha kuwa ukifanya ziara ya kushtukiza mashuleni ni asilimia 47% ya walimu waliopo shuleni ndiyo waliopo darasani kufundisha vipindi walivyopangiwa.

Aidha, walimu wanatumia nusu tu ya muda wanaopaswa kufundisha.


Matokeo yake ni kwamba asilimia 50% ya muda wa watoto shuleni unapotea bila kusoma.

Kiuchumi maana yake ni kwamba tunapoteza asilimia 50 ya uwekezaji katika elimu ukizingatia kwamba pesa nyingi katika elimu zinaenda katika mishahara ya walimu.

Utafiti ambao umetolewa leo uitwao Tanzania Service Delivery Indicators unathibitisha kuwa 49% tu ya Walimu wanaingia darasani na kufundisha, zaidi ya nusu hawapo shuleni kabisa au hawafundishi.

Utafiti huu umehoji walimu 3,692 na wanafunzi 4,041 na umefanywa na REPOA pamoja na Benki ya Dunia.


Mheshimiwa Spika, Hali Hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na motisha na usimamizi hafifu kwa walimu.

Hivyo ni muhimu kufanya bidii kama nchi kutoa motisha kwa walimu.

Lakini ni muhimu pia walimu wasimamiwe na wapewe mafunzo kazini ya mara kwa mara.

Kwa sasa ni 5% tu ya walimu wanakwambia wamewahi kuhudhuria mafunzo yoyote kazini katika miaka mitano iliyopita!!


Ndiyo maana tumekuwa tukidai kwa miaka mingi sana Chombo cha kitaaluma cha Walimu (Teachers’ professional board) lakini serikali imegoma ikiogopa kunyang’anywa udhibiti wa walimu.

Tuwekeze kwa Mwalimu kama ninavyoshauri hapa chini.


Mheshimiwa Spika, Elimu ya Juu nayo ni balaa kabisa.


Ubora wa vyuo vikuu umeanza kutia shaka. Katika utafiti wa juzi juzi wa Times Higher Education, hakuna chuo hata kimoja cha Tanzania kilichopo katika orodha ya vyuo bora 30 Afrika! Tupo nyuma ya Vyuo Vikuu vya Makerere na Nairobi ambavyo tulikuwa tunavizidi Zamani.


Sababu Kubwa ya Kushuka Kwa Ubora wa Vyuo Vyetu Ni Kuwa Hatufanyi uwekezaji katika tafiti. Nchi ilishaamua kuwekeza asilimia moja ya pato la taifa katika utafiti lakini hadi sasa serikali imetoa 0.001%.

Vitabu vya Bajeti vinaonyesha kuwa Bajeti kubwa ya Elimu inakwenda Elimu ya Juu lakini kwenye mikopo. Uwekezaji kwenye Utafiti haufanyiki na tutaathirika sana kama Taifa.


Mheshimiwa Spika, nini falsafa ya Rais Magufuli katika Elimu? Rais anasema ‘ Tanzania ya Magufuli ni Tanzania ya Viwanda’.


Viwanda kwenye nchi ya Wajinga? Nani atafanya kazi kwenye viwanda hivyo? Nani atasimamia mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii na hata ya kisiasa yatakayoletwa na Uchumi wa Viwanda?

Tunaposema tunataka nchi ya uchumi wa kati tunajua mahitaji ya Elimu ya Uchumi wa Kati? Tunaelekeza rasilimali fedha katika kujenga rasilimali watu itakayoendesha uchumi wa Viwanda?


Tunaposema Uchumi wa Viwanda tunawasemea watoto wetu, hatujisemei sisi. Tunasemea kizazi kijacho. Tunakiandaa kwa Tanzania hiyo.


Mheshimiwa Spika, kuna mahusiano chanya kati ya Elimu na ukuaji wa uchumi. Vile vile kuna mahusiano chanya Kati ya ubora wa rasilimali watu ( elimu na afya ) na ukuaji wa Uchumi.

Tafiti zinaonyesha kuwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinaweza kwenda kwa kasi kiuchumi iwapo zitawekeza kwenye Elimu na Afya. Robo ya kasi ya ukuaji uchumi inaweza kuchangiwa Kwa ubora wa Rasilimali Watu pekee.


Hivyo, tunapotaka kujenga Uchumi wa Viwanda na ili uchumi huo uwe na maana ni lazima kuwekeza vya kutosha kwenye Elimu.

Hata hivyo ni lazima tuwekeze tukiwa Na ushahidi wa kisayansi kuhusu nyufa za elimu ya Tanzania (evidence based policy interventions).


Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya Elimu ya Ufundi peke yake inahitaji Watanzania wenye ujuzi wa juu milioni Tatu ifikapo mwaka 2025.

Pia Tanzania inahitaji watu wenye ujuzi wa ufundi (kutoka VETA na Technical Schools) wapatao milioni 7 ifikapo mwaka 2025.


Ni muhimu sana kufungua macho na kufanya maamuzi mahususi kuhusu Elimu. Tunahitaji uwekezaji wa angalau 20% ya Bajeti yetu kwenda kwenye Elimu kwa miaka 10 ijayo ili kuweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye Elimu.

Hata hivyo, kipimo cha msingi cha mafanikio katika mfumo wa elimu ni kama watoto wanaotoka kwenye mfumo huo wa Elimu wana maarifa, ujuzi na uwezo kwa ulimwengu watakaoukabili.


Hatuwezi kupata mafanikio haya bila kufumua mfumo wetu wa Elimu, kupanua demokrasia ya utoaji Elimu na kuhakikisha walimu wanapata motisha.

Moja ya motisha tunayoweza kupawa Walimu ni kuwalipa vizuri, kuwasimamia vizuri na kuwapa mitihani maalumu kila wakati ili kuwapandisha madaraja.


Napendekeza ‘salary scale ya Walimu’ iwe sawa na angalau nusu ya salary scale ya Wabunge na viwango vya mishahara kati ya Walimu wanaofundisha ngazi yeyote ile iwe sawa kulingana na usawa wa elimu, muda kazini na juhudi ( performance based remunarations).


Najua haya yanaweza kuonekana magumu lakini naamini maneno aliyoyema mwanaharakati wa Elimu Nchini Rakesh Rajani aliyepata kusema “More of the same won’t cut it anymore”. Kama Elimu ndio silaha kubwa ya kuleta maendeleo, ni lazima tufanye tofauti ili kuboresha Elimu.


Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwamba Taifa liunde Tume ya Wataalamu ili kuweza kutafuta Nyufa za Elimu yetu na kutoa mapendekezo yanayotokana Na ushahidi wa kisayansi. Tuunde Tume ya Elimu sasa ili tuweze kuwa na muda wa kutosha wa kutatua changamoto za Elimu nchini.


Mheshimiwa Spika, katika pendekezo la kuanzisha Vyuo vya Ufundi kila mkoa natoa maombi maalumu kwa mkoa wa Kigoma kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji (UjijiInstitute of Technology – UIT).

Mji wa Ujiji ni moja ya miji mikongwe nchini ambayo inasinyaa kama sio kufa. Uanzishaji wa Chuo utakaowezesha kudahili angalau wanafunzi 5000 itakuwa ni chachu kubwa ya Maendeleo Mji huu na Tanzania kwa ujumla.


Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji itaweza kusaidia sana kuziba mianya ya wataalamu wa katika kwenye sekta ya usafirishaji (Logistics) kwa kuzingatia kuwa Kigoma ni Lango la Magharibi la Taifa letu.

Napendekeza kuwa Serikali ilitazame kwa kina ombi hili ili kuweza kuongeza wataalamu wa kati katika nchi yetu.


Mheshimiwa Spika, ninapendekeza pia Serikali itazame upya suala la Sera ya Vitabu ili kuhakikisha kuwa uwekezaji katika uchapishaji unaongezeka nchini.

Nadhani ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ubora wa vitabu badala ya yenyewe kuhangaika na kuandika na kuchapisha vitabu. Sera ya Vitabu inazalisha ajira kwenye nchi na inawezesha Watanzania kutafuta fursa kwenye maeneo hayo pia.

Wachapishahji wa ndani wanashindwa kukua kwa sababu Serikali imewabana.


Serikali haipaswi kubana inapaswa kuchochea ukuaji wa sekta ya uchapishaji. Vilevile, napendekeza sana tuwekeze kwenye maktaba za kijamii kwenye kata zetu na miji yetu.

Maktaba hizi ziwe na vitabu na tuhamasishe watu wenye vitabu kutoa vitabu kwa maktaba hizi.

Tujenge Taifa la wasomaji kwa kuhamisha usomaji kuanzia ngazi ya chini kabisa.
Mheshimiwa Spika, nasisitiza kuwa mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu namna ya kutoa mikopo na kuikusanya yachukuliwe kwa uzito unaostahili.

Mikopo isiwe sehemu ya Bajeti ya Wizara badala yake Bodi ipewe fedha moja kwa moja kutoka Hazina ( Direct Transfer ) na mfumo wa malipo udhibitiwe.


Ni lazima tufanye tafiti kuhakikisha kuwa ifikie wakati Bodi ya Mikopo iweze kujiendesha yenyewe kutokana na fedha zinazorejeshwa.

Mfumo wa kutumia Credit Reference Bureau na Vitambulisho vya Taifa na hata mobile technology kuhakikisha mikopo inarejeshwa ni mfumo ambao utakuwa na mafanikio makubwa sana. Serikali ifanyie kazi pendekezo hili.


Mheshimiwa Spika, nasisitiza pia kuwa pendekezo la Kamati kuanzisha President Magufuli Scholarship Award lianze mara moja.

Tuchukue watoto waliofanya vizuri angalau 50 kila mwaka na kuwasambaza kwenye Vyuo Vikuu vikubwa Duniani.

Ndani ya Miaka 10 tutakuwa tumetengeneza mamia ya Watanzania wenye uwezo mkubwa kwenye Nyanja zote nchini.

Rais atakuwa ameacha jambo kubwa na la kukumbukwa.


Zitto Kabwe Ruyagwa
Mei 27, 2016

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

One thought on “Mchango wa Ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto katika Bajeti ya Wizara ya Elimu 2016/17

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.