Elimu bure haimaanishi Elimu bora

13321758_1063115370429624_7116737177068346199_n
Hivi karibuni Serikali ilianzisha utoaji wa elimu bure katika elimumsingi yaani kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne ikiwa ni utekelezaji wa sera mpya ya elimu iliyozinduliwa 2014. Utekelezaji wa sera hii umepokewa kwa shangwe na wazazi kwani umetua mzigo wa ada na michango mingine iliyokuwa ikihitajika shuleni.
Lakini wazazi tukiwa tunashangilia ‘elimu bure’ ambayo bado utekelezaji wake ni changamoto, upande wa ubora wa elimu vipi tunaujua ipasavavyo? Ukweli ni kwamba hali ya ubora wa elimu ni mbaya sana Tanzania na inahitaji suluhisho la haraka. Je ubora katika elimu ni nini?
Ripoti ya Dunia ya Ufuatiliaji wa Ubora (Global Monitoring Report, 2005 p.17) imetoa kanuni mbili za kufafanua maana ya ubora katika elimu. Kanuni ya kwanza ni kwamba lazima elimu itolewayo ilenge kumuendeleza mwanafunzi kupata maarifa sahihi ya kile anachojifunza.
Kanuni ya pili ya elimu bora ni ile yenye kujenga na kuhamasisha thamani na tabia ya mwananchi anayewajibika, mbunifu na mwenye fikra tunduizi. Pia lengo namba sita la Ripoti ya Utekelezaji ya Dakar linasisitiza uhitaji wa kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji yaani mbinu za kufundisha na kujifunza kwani ufundishaji na ujifunzaji ndio unasababisha ubora wa elimu kupatikana. Ni katika ufundishaji na ujifunzaji darasani kati ya mwalimu na mwanafunzi ndipo ubora wa elimu hupatikana; kuna uhusiano mkubwa katika ufundishaji na matokeo ya mtoto shuleni.
Kama ubora wa elimu unapatikana katika kufundisha kwa walimu na kujifunza kwa wanafunzi, je Tanzania hali ikoje? Walimu wana motisha na wanafundisha ipasavyo? Je, watoto wanasoma inavyotakiwa? Mwaka jana 2015 nilipata nafasi ya kutembelea wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na kubaini hali mbaya ya elimu kiasi cha kujihoji ni nini hatma ya walimu na wanafunzi ambao kwa kuwatazama tu wanapata elimu kwa mateso makali.
Katika shule nne za msingi nilizotembelea, shule ya Nansole na Murutanga nilikuta walimu wanaishi ndani ya vyumba vya madarasa, walimu wakuu walinieleza kuwa nyumba za walimu hazitoshi. Nikajiuliza motisha ya mwalimu kufundisha kwa mazingira yale ataipata wapi? Mwalimu hana faragha na familia yake kwani muda wote watoto wanapita na kelele, hawezi kupika wala kuanika nguo zake kwa uhuru. Mazingira kwake yanaathiri ufundishaji wake kwani hana motisha.
Ripoti ya Viashiria vya utoaji wa elimu ya Benki ya Dunia kwa kushirikiana na taasisi ya REPOA na AERC iliyozinduliwa tarehe 27 Mei , 2016 imebainisha kuwa asilimia 37 ya walimu waliopo shuleni hawaingii madarasani, pia asilimia 14 ya walimu hawapo shuleni kabisa. Maana yake ni kuwa wanafunzi hawafundishwi nusu ya vipindi vyote wanavyotakiwa kufundishwa kila siku shuleni.
Shirika la HakiElimu pia liliwahi kufanya utafiti mwaka 2014 ili kuangalia kama walimu wanafundisha ipasavyo? Matokeo ya utafiti huo pia yalionesha kushabihiana na hali hii mbaya katika ufundishaji nchini. Hali hii ya ufundishaji inadhihirisha bayana. Hali duni ya elimu nchini kiasi cha kuhoji elimu bure kama itatoa majawabu ya changamoto hizo.
Hali ya kujifunza kwa watoto pia ni janga la taifa, kwani ripoti hiyo ya Benki ya Dunia imeonesha changamoto kubwa ya miundombinu na ukosefu wa zana za kujifunzia, ambapo asilimia 41 tu ya watoto ndio wana miundombinu mizuri ya kujifunzia kama madarasa na madawati; asilimia 61 pekee ndio wana vitabu. Ni ukweli usiopendwa kuzungumzwa kuwa watoto wengi hawajifunzi wakiwa shuleni. Mazingira ya kujifunzia yanaathiri upatikanaji wa elimu bora na endapo hili halitarekebishwa ubora wa elimu utaendelea kuwa duni.
Ufundishaji na ujifunzaji mbovu darasani huathiri ubora wa elimu. Tukitumia kipimo cha matokeo ya mitihani ya kitaifa kupima ubora wa elimu, hali bado ni mbaya bado hatujaweza kufikia ufaulu kwa asilimia 70 kutoka kwa mwaka 2012. Maana yake ni kwamba hali ni mbaya katika utoaji elimu Tanzania inayohitaji hatua za dharura kuitatua. Ripoti ya HakiElimu ya mwaka 2015 iliyotathmini Miaka 10 ya Rais Kikwete katika elimu pia imebainisha kuwa ubora wa Elimu katika kipindi chake cha uongozi umekuwa mbaya zaidi tangu tupate uhuru mwaka 1961.
Kwa maelezo hayo inatupasa tuzungumze ukweli, bila kuoneana haya kuwa ubora wa elimu nchini ni taabani na tunahitaji kuchukua hatua za haraka kuboresha. Kutangaza elimu bure pekee haitoshi kuinua ubora wa elimu; tunahitaji uwekezaji ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuinua ari ya ufundishaji kwa walimu. Ili kufanya hivyo bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu inapaswa kuongezwa ili kukidhi changamoto zilizopo. Katika miaka mitano iliyopita uwiano wa bajeti ya maendeleo ulikuwa asilimia 11 hadi 16 tu wakati ile ya matumizi ya kawaida ni asilimia 80 hadi 90.
Kiasi hicho hakitoshi kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Tukumbuke ‘Elimu bure’ haimaanishi ‘Elimu bora’.
Mwandishi wa makala ndugu Peter Letema ni afisa kutoka shirika la HakiElimu anapatikana kupitia barua pepe; media@hakielimu.org

HAKIELIMU·THURSDAY, JUNE 23, 2016

Author: Sir Gunda

A Friend of Education

5 thoughts on “Elimu bure haimaanishi Elimu bora

  1. Ntaunga mkono kwa % zote, pia napenda kuongezea kuwa jamii pia unayo wajibu wa kufanya kuonesha uthubutu wao ktk kuchangia ktk ELIMU kwa hali na Mali, sio kila kitu wssubiri serikali wakati ELIMU ipi kwa manufaa yao wenyewe. Mf shule flan hapa nilipo tangu ianzishwe mwaka 2015 haina vyooote vya walimu. Wakiambiwa wakitolee hata kwa nguvu kazi wanadai shule ni ya Mkurugenzi na serikali hivyo watumishi kushare vyoo na wanafunzi?! Jamii za ukanda wa Tanganyika huku uvinza kigoma ni tatizo kubwa saaaana.

    Like

Usikae kimia sema kitu juu ya nukuu hizi

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.