Swali na Jibu | Kunasihi (NECTA 2008)

Taja mambo matatu (3) ya kuzingatia katika kikao cha kunasihi. (NECTA 2008)

 1. Mahali pa kukutana lazima pawe pa faragha.
 2. Wakati wa mazungumzo, mshauri na mshauriwa wakae katika hali ya mazungumzo.
 3. Mshauri ajitahidi kumweka mshauriwa katika hali ya kujiona yupo huru.
 4. Mshauri atumie lugha anayoielewa mshauriwa.
 5. Muda wa mazungumzo upangwe kwa busara ili mshauriwa asipate shida ya kuhudhuria, na afikapo apate muda wa kutosha wa kuzungumza.
 6. Muda wa kuzungumza usiwe mfupi mno au mrefu mno kwani yaweza kuchosha na kupoteza muda.

Swali na Jibu | Umuhimu wa Ushauri nasaha (NECTA 2004)

Eleza umuhimu wa kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wa shule ya msingi, hususani wale wenye matatizo ya kielimu na kifamilia. (NECTA 2004)

1)      Husaidia wanafunzi kujielewa kulingana na hali walizonazo ili kuwasaidia.

2)      Huongeza utambuzi wa mwanafunzi wa nafsi yake kuhusiana na wengine.

3)      Husisitiza mahusiano kati ya matakwa ya kielimu na maendeleo ya binafsi.

4)      Hukuza utambuzi bora wa mwanafunzi kwa familia yake.

5)      Hutoa/huwezesha hisia za usalama na namna ya kuishi kwa amani katika familia.

6)      Huongeza jitihada za mwalimu katika kusaidia matatizo ya watoto.

UALIMU NECTA 2012 | SWALI NA JIBU

944185_552128748171285_1507787981_n

1.       Orodhesha adhabu nne zinazoweza kutolewa na Tume ya Walimu Tanzania kwa mwalimu anayekiuka maadili ya kazi ya ualimu (NECTA 2012)

 • Kufukuzwa kazi na kusimamisha uanachama wake katika utumishi,
 • Kupunguzwa kwa mshahara wake lakini sio chini ya kiwango cha kwanza katika ngazi aliyoajiriwa nayo,
 • Kuteremshwa daraja,
 • Kusimamisha au kuchelewesha nyongeza ya mshahara,
 • Onyo au karipio kali;

Ushauri na Unasihi

308577_10201144942332246_1431798451_n

Eleza kwa kifupi tofauti kati ya Unasihi na Ushauri? (NECTA 2008)

Ushauri huwa na lengo la kuzuia tatizo lisitokee, hivyo mara nyingi ushauri hutolewa kabla ya tatizo kutokea. Wakati wa ushauri, mteja (mshauriwa) huwa ni mpokeaji tu wa ushauri toka kwa mtoa ushauri. Mshauri anaweza kuwa ni mtu yeyote. Hivyo kwa ujumla, Ushauri hutolewa kwa mtu yeyote.

Nasaha hutolewa baada ya tatizo kuwa limetokea. Mara nyingi nasaha hutolewa kwa lengo la kutibu au kupunguza uwezekano wa tatizo lililopo kutokea tena au kumfanya mwenye tatizo akubaliane na hali halisi kuwa analo tatizo na kuangalia namna ya kukubaliana na kukabiliana nalo. Wakati wa Unasihi, mtoa nasaha (Mnasihi) na mteja (mnasiwa) hubadilishana mawazo na si mpokeaji tu wa kile kinachopendekezwa na mnasihi. Unasihi hutokana na kujifunza na kuwa mtaalamu wa kutoa nasaha.Hivyo, unasihi hutolewa kwa mtu mwenye tatizo tu.

Makazi ya Maarifa | Nadharia za Kujifunza

1015201_536685933034785_446464760_o

Fafanua vipengele sita (6) vya Makazi ya Maarifa kama vilivyoainishwa na mwanasaikolojia Benjamin Bloom.

1)      Kumbukumbu

 • Uwezo wa mwanafunzi kukumbuka maarifa aliyoyapata.
 • Mwanafunzi anaweza kutaja, kuonesha, au kueleza kwa kifupi juu ya kile alichojifunza.
 • Hapa mwanafunzi anaweza kutaja jambo fulani alilojifunza bila kuwa na maelezo ya kutosha juu ya jambo hilo.

2)      Ufahamu

 • Mwanafunzi anaweza kusoma jambo fulani na kuelewa dhana yake halafu anaweza kuunda maelezo yake binafsi tofauti na yaliyotolewa mwanzo bila kuathiri maana ya dhana hiyo.
 • Mwanafunzi anaweza kutafsiri kanuni, kufupisha habari, kutumia habari kujibu maswali, kutoa sababu juu ya mada fulani.

3)      Matumizi

 • Ni uwezo wa kutumia mambo au maarifa aliyojifunza katika mazingira mengine au katika hali halisi.
 • Mfano, kufumbua mafumbo ya kihisabati kwa kutumia kanuni za kawaida za hesabu, kutumia maarifa aliyojifunza kutatua matatizo ya kimaisha, kukokotoa mahesabu kwa kutumia kanuni, kufundisha darasani kutumia njia/mbinu alizojifunza kwenye somo la ufundishaji, kutumia kanuni fulani ya hisabati kukokotoa na kutoa jawabu.

4)      Uchambuzi/Uchanganuzi

 • Ni uwezo wa kujadili kwa kina na kutoa maoni kuhusu jambo fulani la kitaaluma.
 • Mwanafunzi anaweza kuwa na maelezo mengi kuhusu jambo moja linaloelezwa au kujadiliwa mfano, anaweza kutoa faida na hasara au anaweza kulinganisha dhana.

5)      Uundaji

 • Ni uwezo wa kujadili kwa kina mambo mbalimbali na kuyaweka pamoja.
 • Mwanafunza anaweza kuunganisha mambo mbalimbali kuwa kauli ya aina moja na inayoeleweka, kujenga hoja kulingana na mawazo mengi aliyonayo na kutoa hitimisho kutokana na yale yaliyozungumzwa.

6)      Tathmini

 • Ni uwezo wa kuthamanisha mafanikio au thamani ya kazi au jambo.
 • Mtoto anaweza kuthamanisha matukio, maelezo au tabia fulani na kusema ni nzuri au mbaya kiuhalisia.

Maswali na Majibu – Sehemu I | Dhana ya Ualimu

DSC01466

1.       Fafanua dhana nne (4) za ualimu.

a.       Dhana ya Maelezo

Kulingana na dhana hii, ualimu ni utoaji wa maarifa na ujuzi.

b.      Dhana ya Mafanikio

Katika dhana hii kufundisha na kujifunza ni muhimu; hii ina maana kwamba kufundisha hakuwezi kukawepo bila kujifunza kuwepo.

c.       Dhana ya Makusudio

Katika dhana hii, tendo la kufundisha linahusisha kutambua umuhimu wa malengo, mawazo, na imani ya mwalimu kuwa ni vigezo muhimu katika utendaji wake wa kazi. Smith (1989) anasisitiza kuwa imani hizo ni muhimu sana katika kuleta athari katika kazi ya ualimu.

d.      Dhana ya Kisayansi

Kulingana na dhana ya kisayansi ualimu huoneshwa kwa mafanikio au athari. Ualimu hujumuisha vipengele vya uwezo wa kuleta mafanikio. Mafanikio ya ualimu ni kubadilika kwa mwanafunzi kimaadili, kiujuzi na kifikra. Ualimu usioleta au kuonesha mafanikio mema una kasoro.

2.       Taja sifa zinazomfanya Mwalimu kuwa kisima cha maarifa na ujuzi.

Sifa zinazomfanya mwalimu kuwa kisima cha maarifa na ujuzi ni;

 • Mwalimu ana utaalamu wa kumuwezesha mtoto kuanza kuhesabu, kusoma na kuandika;
 • Baadaye mwalimu humfundisha mwanafunzi maarifa ya jamii, hisabati, stadi za kazi, sayansi, afya, lugha na taaluma mbalimbali.

3.       Eleza jinsi utakavyowasaidia wanafunzi wako ambao idadi yao ni kati ya 70 – 90 wakiwa katika chumba kimoja cha darasa.

Yapo mambo mengi ambayo mwalimu anapaswa kuyafanya ikiwa ni pamoja na;

 • Kugawa wanafunzi katika vikundi ili wasome kwa zamu
 • Kutumia mbinu ya kazi mradi zaidi katika kufundisha na Kuwapa kazi nyingi za kufanya darasani za kujisomea;
 • Kufundisha kwa kuzunguka zunguka darasani kuliko kukaa mbele tu ya darasa kwani wanafunzi wengi hasa wa nyuma darasani hawawezi kusikia vizuri.

4.       Ni vipengele vipi vinavyothibitisha kushuka kwa hadhi ya walimu?

 • Kuwapa wanafunzi mimba;
 • Kulewa ovyo;
 • Kutumia lugha chafu mbele ya wanafunzi;
 • Kuvaa ovyo ovyo;
 • Kushindwa kufundisha vizuri;
 • Kushindwa kuongea kiingereza;
 • Kutojua kikamilifu maarifa ya masomo mengi na Kuuza mitihani

5.       Ni mambo gani muhimu hufanyika katika vyuo vya ualimu (Daraja A) yanayohusika na kumwandaa mwalimu tarajali wa shule za msingi?

 • Hufundishwa masomo ya Saikolojia, Falsafa ya Elimu, Msingi ya Elimu, Mitaala na Ufundishaji na Njia mbalimbali za kufundisha masomo;
 • Hujifunza kuandaa maazimio ya kazi na maandalio ya somo;
 • Hujifunza taratibu, sheria na miiko ya kazi;
 • Hufanya Mazoezi ya kufundisha.

6.       Eleza kwa kifupi changamoto nne zinazoifanya kazi ya ualimu hapa Tanzania ionekane ni kazi ngumu na isiyo na mvuto (NECTA 2011).

 • Mazingira magumu na duni ya kufanyia kazi na idadi kubwa ya wanafunzi darasani;
 • Maslahi madogo ya mishahara;
 • baadhi ya watu kujiunga na vyuo vya ualimu bila ya kuwa na sifa hivyo kuongeza mzigo kwa walimu wenzao kazini;
 • walimu wengi huacha kazi na kujiunga na kazi nyingine hivyo kuwakatisha tama walimu wengine;
 • ukosefu wa vifaa vya kufundishia na uhaba wa samani madarasani;
 • ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kazini.

7.       Orodhesha adhabu nne zinazoweza kutolewa na Tume ya Walimu Tanzania kwa mwalimu anayekiuka maadili ya kazi ya ualimu (NECTA 2012)

 • Kufukuzwa kazi na kusimamisha uanachama wake katika utumishi,
 • Kupunguzwa kwa mshahara wake lakini sio chini ya kiwango cha kwanza katika ngazi aliyoajiriwa nayo,
 • Kuteremshwa daraja,
 • Kusimamisha au kuchelewesha nyongeza ya mshahara,
 • Onyo au karipio kali;

8.       Eleza kwa ufasaha sababu tano (5) zinazofanya ualimu uwe kazi ya kitaalamu (NECTA 2012).

 • Utaalamu hutoa huduma kwa jamii
 • Una miiko ya kazi – Utaalamu una miiko ya kazi ambayo hueleza kinaganaga uhusiano kati ya mtaalamu na mteja wake ambayo inamlinda mteja. Katika Tanzania Tume ya Utumishi wa Walimu inaeleza miiko katika kazi ya walimu na pia Chama cha Walimu kinasisitiza kimsingi udumishaji wa miiko ya walimu kazini.
 • Una utaratibu unaofahamika wa kumwendeleza mfanyakazi – kila kazi ina namna yake ya kutoa mafunzo kazini. Katika ualimu kumekuwa na mafunzo ya aina mbalimbali ya kumwendeleza mwalimu.
 • Una utaratibu mahsusi wa mawasiliano – kuanzia ngazi ya chini kabisa mwalimu anautaratibu mahsusi wa mawasiliano kuanzia kwa mwalimu mkuu hadi waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi.

9.       Eleza sifa tatu (3) za mwalimu zinazoweza kumfanya aheshimike kwa wanafunzi na wanajumuia.

 • Ana dumisha miiko na maadili ya kazi yake ya ualimu;
 • Anaipenda kazi yake na kufundisha kwa moyo;
 • Hujitolea katika kuisaidia, kuishauri na kushiriki katika shughuli za maendeleo katika jamii

10.   Eleza umuhimu wa mafunzo ya ualimu kazini kwa walimu walio kazini.

Mafunzo ya ualimu kazini husaidia;

 • Kuziba mapengo yaliyoachwa na mafunzo tarajali;
 • Kupata maarifa mapya na mabadiliko ya kielimu na kijamii yanayotokea nchini na duniani kote;
 • Kuelewa mabadailiko ya mitaala pamoja na mihtasari;
 • Kusahihisha makosa yanayotokea katika vitabu na mihtasari;
 • Kuenda na wakati katika kuelewa mbinu za kufundishia;
 • Kujifunza mbinu za utawala wa shule.

Makuzi ya Mtoto | Sehemu ya I

Ili kuelewa zaidi makuzi ya mtoto kiakili, Mwalimu yampasa kufahamu vizuri jinsi mwili wa mtoto unavyokua na kukomaa.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya kukua kwa akili na kukua kimwili kwa mtoto. Mwalimu shuleni hushughulikia zaidi kukua kwa akili ya mtoto.

wanafunzi

Vipengele vya Kukua kwa Mtoto

Kama mwalimu ni vyema zaidi kuelewa jinsi kukua kimwili kwa mtoto kunavyohusiana na kukua kiakili.

1. Kukua Kimwili

Ni ongezeko la ukubwa wa umbo la mwili na viungo vyake. Baadhi ya sehemu za mwili hufifia na kupote mfano nywele za utotoni na kitovu. Vitu vingine pia hujitokeza katika mwili kwa mfano ndevu kwa wanaume na matiti kwa watoto kwa kike.

Ukubwa wa ubongo huongezeka, mifupa  na kukomaa kwa misulu na neva za mwili.

2. Kukua Kiakili

Ukuaji wa akili wa mtoto huongezeka na kumuwezesha kuweza kukabiliana zaidi na mazingira anamoishi hatua kwa hatua. Uwezo huo hutegemea upevukaji na utayari wa viungo vya mwili kama vile kukomaa kwa ubongo, neva na misuli ya mwili.

3. Kukua Kimaono

Hii ni hali ya kuongezeka uwezo na hisia za mwili. Ni kujitambua kwa mtoto, kama vile kupenda, kuchukia, kuona wivu, ubinafsi, kukasirika, kukasirika na mengine. Matendo haya hukomaa zaidi kadri mtoto anavyokua kimwili na kiakili pia.

4. Kukua Kijamii

Aidha hii ni hali ya mtoto kuongezeka uwezo wa kutenda yale yanayotakiwa na jamii inayomzunguka. Kukua Kijamii ni;

 • kukua kimaadili,
 • kuongezeka uwezo wa kuishi kufuatana na utamaduni, mila na desturi za jamii inayohusika,
 • mtoto kutambua ni lipi linakubalika na jamii na lipi lisilohusika.

TET

Jipime na Msawali 50 Kusherehekea Muhula Mpya 2014 | Maswali Mchanganyiko

 1. Mbinu za kufundishia ni nini?
 2. Elimu ya awali ni nini?
 3. Eleza umuhimu na mapungufu ya Mtaala wa elimu Tanzania.
 4. Bainisha misingi ya kufanya upimaji wa kielimu
 5. Bainisha misingi ya kufanya tathmini ya mtaala
 6. Dhana ya lugha hujipambanua katika sura kuu tano. Taja sura kuu nne za lugha.
 7. Utajuaje kuwa tendo la kujifunza limekamilika kwa mwanafunzi wako?
 8. Kuna aina ngapi za unasihi?
 9. Taja stadi za kimaadili ambazo mwalimu huzijumuisha katika upimaji wa elimu.
 10. Je, kuna umuhimu gani wa mpango wa elimu hapa Tanzania?
 11. Onesha utaratibu wa uendeshaji wa elimu nchini Tanzania kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995.
 12. Je, umewahi kuuona mtaala wa shule ya msingi? Kama siyo kuna dosari gani ya kutouona mtaala huo?
 13. Tofautisha kati ya Utawala na Uongozi.
 14. Kwa kutumia mchoro onesha mtiririko wa Muundo wa uongozi chuoni.
 15. Nini maana ya Elimu ya watu wazima?
 16. TEHAMA ni nini?
 17. Fafanua dhana ya kusoma na kuandika.
 18. Eleza kwa kifupi maana ya Kisomo Chenye Manufaa (KCM) na Kisomo cha Kujiendeleza (KCK).
 19. Mwanafunzi mtu mzima ni nani?
 20. Fafanua dhana ya Elimu.
 21. Kujifunza kwenye maana kuna maana gani?
 22. Kwa kutumia mifano mitatu eleza maana ya kujifunza kipurure.
 23. Eleza kwa maneno yako mwenyewe maana ya “Uhawilishaji wa Maarifa”.
 24. Eleza kwa kutoa mifano maana ya uhawilishaji ulalo na uhawilishaji wima.
 25. Kuvia akili ni nini?
 26. Eleza mahitaji ya mwanafunzi katika umri wa  kuanzia miaka 7 – 15.
 27. Kwa nini mwanafunzi hufundishwa stadi ya kuzungumza kabla ya kumfundisha stadi ya kuandika?
 28. Maarifa ni nini?
 29. Eleza na fafanua nadharia ya “Umwenendo”.
 30. Eleza maana ya usemi huu, “Motisho huongeza tija”.
 31. Nini umuhimu wa Elimu ya Maadili katika kujifunza?
 32. Kichocheo hasi hutolewaje?
 33. Kuna aina ngapi za motisho?
 34. Taja mambo yanayoonesha kuwa mwanafunzi amejifunza.
 35. Kuna manufaa gani kwa mwalimu kuwapa wanafunzi kazi za kufanya nyumbani?
 36. Eleza na fafanua misingi inayotumiwa wakati wa kutoa mazoezi.
 37. Tunga maswali matano (5) yanayopima ngazi ya juu ya maarifa.
 38. Taja aina tano (5) za zana unazoweza kutengeneza kutoka mazingira ya shule.
 39. Eleza manufaa ya kutumia zana wakati wa kufundisha.
 40. Taja na eleza aina mbalimbali za mbao za kufundishia.
 41. Eleza maana ya dhana. Toa mifano kusaidia ufafanuzi wako.
 42. Eleza hatua za kufuata wakati unapotaka kutatua tatizo lolote.
 43. Ubora wa njia yeyote unategemea mambo gani?
 44. Mwanafunzi anaweza kujifunza bila kuwapo kwa mwalimu. Eleza ni katika mazingira gani hali hii inaweza kutokea.
 45. Kwa mujibu wa Hurlock michezo ni nini?
 46. Jadili hitilafu tatu (3) za kuzungumza wanazopata watoto.
 47. Eleza kwa kifupi kuhusu mitihani ya insha.
 48. Eleza majukumu manne (4) ya Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC).
 49. Taja faida tano (5) za maswali yanayoulizwa na mwalimu darasani.
 50. Kujifunza huimarika kwa kuzingatia Nyanja kuu tatu (3), zitaje.

 

Maswali na Majibu ya Ualimu 2013 | Tafakari na Furahia Christmas na Mwaka Mpya 2014

1. Ni mambo gani muhimu hufanyika katika vyuo vya Ualimu daraja “A” yanayohusika na kumwandaa mwalimu tarajali wa shule za msingi?

 • Hufundishwa masomo ya saikolojia, falsafa ya Elimu, Misingi ya Elimu, Mitaala na ufundishaji na Njia mbalimbali za kufundisha masomo;
 • Hujifunza kuandaa maazimio ya kazi na maandalio ya somo;
 • Hujifunza taratibu, sharia na miiko ya kazi,
 • Hufanya mazoezi ya kufundisha.

2. Kwa nini saikolojia ni taaluma ya sayansi?

Kwa ujumla saikolojia ni taaluma ya kujifunza tabia na mwenendo wa viumbe, ni taaluma ya kisayansi kwa kuwa huhusika na kujifunza na kupambanua kwa undani mabadiliko ya tabia ya binadamu kutokana na kubadilika kwa vipindi vya ukuaji kwa kiumbe na mazingira anamoishi.

3. Saikolojia ya mtoto ni nini?
Saikolojia ya mtoto ni tawi la elimu linaloshughulikia taaluma ya kujifunza tabia na mwenendo wa mtoto katika hatua mbalimbali za ukuaji wake.

4. Mabadiliko gani yanatokea kwa mtoto kati ya umri wa miaka 2 – 5?
Hiki kinaitwa kipindi cha utoto kwani;

 • Misuli yam tot na neva zake huanza kukomaa na kupevuka,
 • Huanza kufundishwa matumizi ya vitu mbalimbali mfano, choo, kupiga mswaki nk,
 • Huongezeka urefu kwa kasi,
 • Mifupa hukua kwa kasi

5. Lugha ni nini?
Lugha ni chombo cha mawasiliano miongoni mwa binadamu, humsaidia kujenga mahusiano mazuri na wenzake na pia hutumika kufundishia na kujifunza mambo mbalimbali.

6. Taja na fafanua aina kuu tatu za hitilafu ya kuzungumza lugha.

 • Afazia – ni hitilafu katika uwezo wa kutambua na kuelewa maneno yaliyosemwa au kuandikwa na hitilafu katika kubuni maneno ya kuzungumza;
 • Disarthia – ni hitilafu ya kuzungumza inayotokana na mtoto kutoweza kutamka maneno vizuri;
 • Aphonia – hitilafu ambayo mtoto amepoteza kabisa sauti yake.

7. Tofauti ya makuzi na ukuaji wa mtoto
Makuzi kwa mtoto huanza kabla ya kuzaliwa. Mtoto hukaa tumboni mwa mama kwa muda waq miezi tisa au siku kati ya 280 hadi 290 tangu kutungwa mimba. Baada ya kuzaliwa hatua za ukuaji huendelea kwa kupevuka na kukomaa kwa viungo vya mwili.

8. Motisho ni nini?
Katika mazingira ya kujifunza motisho ni kitendo cha kumfanya mwanafunzi ajifunze au awe na ari ya kujifunza. Motisho huhusisha utaratibu wa kutoa vivutio au msukumo Fulani kwa mwanafunzi ili kumfanya ajifunze.

9. Uhawilishaji wa maarifa ni nini?
Ni hali au kitendo cha kutumia maarifa uliyonayo katika kujifunza maarifa mapya.

10. Mtaala ni nini?
Mtaala ni mkusanyiko wa stadi, maarifa na mwelekeo uliopangwa kufundishwa na kujifunzwa na kikundi fulani kwa kipindi kilichopangwa. Pia Mtaala hubainisha kiasi cha maudhui yatakayofundishwa na kujifunzwa na malengo yanayotarajiwa kufikiwa. Maudhui hayo yatakayofundishwa hujitokeza katika muhtasari wa vitendo vya masomo yaliyokubalika.

11. Eleza dhana ya Muhtasari wa somo?
Muhtasari ni mpango wa mambo yaliyopangwa kufundishwa darasani. Pia ni andiko rasmi linalotoa mwongozo wa maarifa, stadi na mwelekeo inayotakiwa kufundishwa kwenye darasa fulani. Mada za muhtasari huonesha mambo ya msingi yanayohusu somo husika. Kwa mfano ujuzi unaotarajiwa kujengwa, malengo mahususi, mada, mbinu za kufundishia na kujifunzia, zana za kufundishia na kujifunzia, upimaji na muda wa masomo kwa wiki.

12. Ni nini tofautisha kati ya Ufaraguzi na Utengenezaji wa zana?
Utengenezaji ni kufanya au kuunda kitu kwa kutumia makunzi halisi. Kutengeneza kunaambatana na michoro, vipimo na makunzi iliyoandaliwa kabla ya uundaji wenyewe kufanyika. Katika utengenezaji muda mrefu unaweza kuhitajika kukamilisha zana unayoitengeneza.
Ufaraguzi ni tendo la ubunifu wa kutengeneza zana papo kwa papo au kutengeneza kwa kutumia makunzi mbadala yanayopatikana katika mazingira husika. Ufaraguzi hauhitaji muda mwingi sana.

13. Vitendeo ni nini?
Ni zana za vitendo vya Elimu ya Awali ambavyo ni vifaa vinavyotumika katika masomo kwa ajili ya kutendea vitendo vya dhana zilizoandaliwa kufundishwa.

14. Orodhesha vitendo sita (6) vya masomo vilivyopo katika muhtasari wa elimu ya awali;

 1. Vitendo vya Hisabati
 2. Vitendo vya Kiswahili
 3. Vitendo vya Sayansi
 4. English learning activities
 5. Vitendo vya Sanaa
 6. Vitendo vya Haiba na Michezo

15. Fafanua uboreshwaji wa Mtaala wa Elimu ya Awali.
Kabla ya uboreshaji wa mtaala wa elimu ya awali wa mwaka 2004, muhtasari wa elimu ya awali ulikuwa na vitendo vya masomo vipatavyo tisa (9) ambayo ni;

 1. vitendo vya Kiswahili,
 2. English learning activities,
 3. vitendo vya michezo,
 4. vitendo vya Hisabati,
 5. vitendo vya Sayansi,
 6. vitendo vya afya,
 7. vitendo vya muziki,
 8. vitendo vya Sanaa na
 9. vitendo vya Haiba.

Baada ya uboreshaji wa mtaala, vitendo vya kujifunza vilipunguzwa hadi kufikia jumla ya vitendo vya masomo sita (6) tu. Mabadiliko hayo yalitokana na kuunganisha vitendo vya Haiba na vitendo vya michezo na kuwa vitendo vya Haiba na Michezo, vitendo vya Muziki kuunganishwa na vitendo vya Sanaa na kuwa vitendo vya Sanaa, vitendo vya Afya viliunganishwa na vitendo vya Sayansi na kuwa vitendo vya Sayansi.

16. Fafanua maana ya Elimu linganishi;
Elimu linganishi ni elimu inayoangalia zaidi mfumo wa elimu moja kutoka nchi moja na kulinganisha na mfumo wan chi nyingine katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo katika jamii hususani kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

17. Fafanua neno “Saikolojia” na orodhesha matawi yake.
Saikolojia ni neno kutoka katika tafsiri ya neno la kiingereza lililotoholewa kutoka lugha ya kigiriki linalotokana na muunganiko wa maneno mawili yaani ‘psycho’ likimaanisha akili na ‘logos’ likimaanisha elimu. Hivyo saikolojia ni elimu inayohusu ubongo na mchakato unaotokea ndani yake na jinsi unavyoathiri tabia za kiumbe. Kwa ujumla Saikolojia ni taaluma ya kisayansi inayoshughulikia tabia na mwenendo wa maisha ya binadamu na wanyama.
Saikolojia ina matawi yake ambayo ni;

 1. Saikolojia ya Kijeshi,
 2. Saikolojia ya Biashara,
 3. Saikolojia ya Kliniki/Tiba,
 4. Saikolojia ya Unasihi,
 5. Saikolojia ya Elimu,
 6. Saikolojia ya Elimu Jamii,
 7. Saikolojia ya Makuzi,
 8. Saikolojia ya Watoto na
 9. Saikolojia ya Viwanda.

18. Sosholojia ni nini?
Sosholojia ni sayansi inayohusiana na tabia ya mtu na jamii yake inayomzunguka. Tabia ya mtu inaweza kubainishwa pale mtu anapokuwa katika makundi ya watu ambamo hujifunza mila, desturi na utamaduni.

19. Orodhesha vigezo kumi (10) utakavyotumia katika kuchagua zana ya kufundishia;
Katika uchaguzi wa zana ya kufundishia na kujifunzia ni muhimu kufuata vigezo, Vigezo hivo ni kwamba zana ni lazima inatakiwa kuwa na:

 1. Uimara
 2. Ukubwa unaofaa
 3. Mvuto na kusisimua fikra
 4. Malengo ya somo yahusiane
 5. Kuhusika kwa wanafunzi katika shughuli za kujifunzia
 6. Urahisi wa upatikanaji katika mazingira unamoishi
 7. Umuhimu na ulazima katika kuleta maana
 8. Rahisi kueleweka kwa mtumiaji mwenyewe
 9. Ubunifu katika kutengenezwa
 10. Mwonekano wa kueleweka katika kujifunza
 11. Rahisi kutafsiri mambo mengi yaliyo halisi

20. Taja sifa tano (5) muhimu ambazo za zana za kufundishia na kujifunzia zinatakiwa kuwa nazo;
Zana za kufundishia na kujifunzia zinatakiwa:

 • Zilete maana na makusudio
 • Ziwe sahihi
 • Inatakiwa ziwe rahisi
 • Zisiwe za gharama
 • Zinatakiwa ziwe kubwa zenye mwonekano kwa wanafunzi walio mbali
 • Ziwe za kisasa na zenye kuvutia kama vile rangi
 • Ziweze kubebeka kirahisi
 • Ziweze kuleta motisha kwa wanafunzi
 • Ziendane na umri wa watoto

Ualimu | Maswali na Majibu

walimu na ualimu

1.       Mwalimu anatumia mbinu gani kukabiliana na tatizo la upungufu wa vitabu vya kiada?

 • Kununua kwa kutumia fedha za miradi
 • Kuagiza wilayani
 • Kuazima shule yenye vitabu vingi
 • Kuwaagiza wanafunzi wanunue
 • Kutoa kivuli (photocopy) cha kitabu kinachokosekana

2.       Eleza sifa za taaluma ya ualimu

 • Ina miiko ya kazi
 • Huhitaji muda mrefu wa kupata maarifa na kufanya mazoezi
 • Utaalamu hutoa huduma kwa jamii
 • Una kiasi kikubwa cha uhuru

3.       Eleza kazi za TSD;

 • Kuendeleza na kusimamia huduma
 • Kumshauri waziri kuhusu uendeshaji na usimamizi wa huduma kwa walimu wote kama itakavyotolewa mara kwa mara katika sheria za utumishi
 • Kusimamia kama chombo cha upatanishi kati ya mwalimu, mwajiri na jumuiya ya wafanyakazi (TFTU) na chama cha walimu Tanzania (CWT)
 • Kuendeleza utaratibu kwa walimu wote walioko kazini
 • Kutekeleza mambo yote yalioelezwa katika kanuni na sheria za utumishi

4.       Ofisi ya Ukaguzi wa shule;

 • Kazi kubwa ya wakaguzi wa shule licha ya kuangalia mahudhurio ya walimu na wanafunzi pia ni kukagua namna ya ufundishaji kwa walimu;
 • Kufuatilia utekelezaji wa mitaala shuleni na kushauri mbinu na vifaa ambavyo walimu wanapaswa kutumia;
 • Baada ya ukaguzi huandaa taarifa na kuipeleka Wizarani au kwa maafisaelimu wa mikoa ikiwa na mapendekezo ya kuondoa dosari zilizojidhihirisha katika mtaala unaohusika.

5.       Bainisha matatizo yanayomkabili mwalimu katika mazingira ya kazi

 • Uhaba au ukosefu wa nyumba za walimu karibu na maeneo yao ya kazi
 • Ukosefu wa usafiri hususani maeneo ya vijijini
 • Idadi kubwa ya wanafunzi darasani
 • Uhaba na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kujifunza
 • Uhaba wa vyumba vya madarasa
 • Ukosefu wa maji safi na salama
 • Ukosefu wa mafunzo kazini ya kumwendeleza mwalimu
 • Hadhi duni na heshima ya mwalimu inavyoonekana katika jamii

6.       Pendekeza njia mbazo mwajiri atazitumia kupunguza changamoto za ualimu katika mazingira ya kazi

 • Kusikiliza malalamiko ya walimu na kuyafanyia kazi
 • Kuwa karibu na walimu na kuwamotisha
 • Kutenga bajeti ya kutosha ili kuhakikisha vifaa muhimu vinapatikana shuleni
 • Kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuleta huduma muhimu karibu na shule mfano Maji
 • Kuwapatia walimu mafunzo ya mara kwa mara kazini ili kuimarisha utendaji wao wa kazi
 • Kuboresha mitaala ya elimu ili kumpunguzia mwalimu mzigo wa kufundisha vitu visivyo na tija kwa wanafunzi

7.       Eleza malengo ya mafunzo ya ualimu chuoni

Mafunzo ya ualimu yana malengo mahsusi yanayoongozwa na dira na falsafa ya elimu nchini. Hapa Tanzania malengo ya mafunzo ya ualimu yamefafanuliwa vyema katika Sera ya Elimu na Mafunzo. Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo (1995), madhumuni na malengo ya elimu ya mafunzo ya ualimu ni;

 • Kuwapa wanachuo nadharia ya msingi ya elimu, saikolojia, unasihi na ushauri
 • Kuwapa wanachuo msingi na mbinu za kufundisha, ubunifu na bidaa
 • Kuinua kiwango cha uelewa wa misingi ya mtaala wa shule
 • Kunoa walimu tarajali, walimu na wanafunzi kimaarifa na umahiri katika baadhi ya masomo, stadi na teknolojia
 • Kuwapa ujuzi na mbinu za upimaji na tathmini katika elimu kuwawezesha wanachuo na walimu wa shule na wanafunzi kupata ujuzi wa elimu na mafunzo ya uongozi na utawala (ETP 1995;5)

8.       umuhimu wa kujiendeleza kitaaluma kwa mwalimu

 • Huongeza maarifa na ujuzi katika mada anayoishughulikia;
 • Kuongeza moyo wa kujiamini na kufanya kazi bila woga;
 • Kuongeza kipato; mwalimu anapohitimu kiwango Fulani cha elimu aidha hupewa nyogeza mbili za mshahara au kupandishwa daraja;
 • Kuongeza hadhi ya mwalimu

9.       Eleza sifa za mwalimu mahiri;

 • Hujiongoza, hujituma na hupenda kazi yake
 • Hutumia mbinu na njia zinazomfanya mwanafunzi amuelewe na kulipenda somo lake
 • Ni mfaraguzi na mbunifu wa vifaa vya kufundishia kulingana na mazingira yake
 • Hulimudu somo na mada anazofundisha
 • Ni mwenye heshima na nidhamu kwa wanafunzi na watumishi wenzake
 • Anapenda kujifunza na kuthamini michango ya wengine juu ya kazi yake
 • Anapenda na kuhimiza ushirikiano na mawasiliano na wadau wengine wa elimu

10.   Ni vipengele vipi vinavyothibitisha kushuka kwa hadhi ya walimu?

 • Kulewa hovyo
 • Kutumia lugha chafu mbele ya wanafunzi
 • Kuvaa ovyo ovyo
 • Kushindwa kufundisha vizuri
 • Kudai hongo
 • Kuwapa wanafunzi mimba
 • Kushindwa kuongea kiingereza
 • Kutokujua kikamilifu maarifa ya masomo mengi
 • Kuuza na kununua mitihani

****************************************************

Walimu na Ualimu tunapenda kuwashukuru wote ambao wamekua wakichangia Ujenzi wa Maktaba ya Jamii kabanga.

Wewe kama Mdau Muhimu karibu sana na tunakuomba uendelee kuchangia kadri Mungu atakavyokuwezesha.

Kiasi cha Shilingi 1,620/= utakua umefanikisha kununua matofali 18 yatakayosaidia kukamilisha ujenzi wa Maktaba ya Jamii kabanga.

Unaweza kuchangia kupitia namba hizi na Mungu Akubariki sana!

 • M-Pesa namba 0767 92 92 96
 • Airtel Money Namba 0786 926285 na
 • Tigo Pesa namba 0714 227875